Mkufunzi wa Mashetani wekundu wa Manchester United Erik Ten Hag huenda akajipata pabaya. Imebainika kuwa anapokea upinzani mkali kutoka kwa nyota kadhaa klabuni hapo hususan baada ya kurushiana cheche za vurugu na Anthony Martial katika mtanango ulioshuhudia Man United wakipokezwa kipigo ugani St James Park na Newcastle United.
Sasa hivi Ten Hag anapambana na upinzani mkali kutoka katika chumba cha kubadilisha sare, huku wachezaji wengi wakionekana kumsuta.Ten Hag aligwaduana vikali na mshambulizi huyo kufuatia kuonyesha utepetevu uwanjani. Halikadhalika, winga Marcus Rashoford alikashifiwa vikali na washabiki wa Man United kwa kuonyesha ulegevu uwanjani. Mara kadhaa alipoteza mpira na kupoteza ari ya kuuwania ili kuurudisha katika himaya yake. Sasa kitendo cha Ten Hag kumfokea vikala Martial na kumwacha Marcus Rashford kumezua maswali mengi yanayohitaji majibu.
Vyombo kadhaa vya habari karibu na klabu hiyo vimethibitisha kwamba wachezaji kadhaa sasa hawafurahishwi na hali ilivyo klabuni hapo. Hili linakuja wakati ambapo Manchester United ina misururu kadhaa ya mitanange mizito ikiwemo Chelsea Leo hii, Bayern Munich Jumanne ijayo katika mtanange ambao Man United ni lazima washinda ikiwa ari na azma yao ni kubakia katika kipute hicho la Ligi Kuu Barani Ulaya, na daadaye waitembee Liverpool ugani Anfield. Michezo hii yote ni muhimu sana kwa Ten Hag kusajili matokeo mema ikiwa nia yake ni kusalia klabuni hapo.
Kuna hofu kwamba hali hii huenda ikaongezeka ikizingatiwa kuwa Man United tayari wamepoteza mechi kumi ( 10 ) kati ya ishirini na moja ( 21 ) walizocheza msimu huu. Mlinzi na mshindi wa kombe la Dunia Rafael Varane tayari amepigwa shoka baada ya kupoteza nafasi yake katika kikosi Cha kwanza klabuni hapo huku winga matata Jadon Sancho akisalia nje baada ya kukataa kumwomna radhi mkufunzi wake.
Si mara ya kwanza mkufunzi Ten Hag kuonyesha ukufunzi wa kimabavu klabuni hapo huku duru zikieleza kwamba anawapendelea wachezaji wengine mazoezini huku wengine akiwaonyesha ukali wake. Wachezaji kadhaa wakiwa tayari wameshaligundua hiki, huendi Ten Hag akauponza kama hatasajiki matokeo mazuri. Chuma chake ki motoni!