Home Careers Mr Bado, Msanii mwenye kipaji cha ajabu!

Mr Bado, Msanii mwenye kipaji cha ajabu!

by Kaka Benayah
3 min read

Wasemao husema kuwa kipaji si ndumba! Anayepeana vipaji ni Mola mwenyewe na atakayepewa hapokonyeki. Naam, akipewa ashapewa. Ni dhahiri shahiri kwamba wapo watu wenye vipaji aina tofauti tofauti.

Binadamu anaweza kuwa na kipaji kimoja ama akawa na vipaji kadhaa. Wingi wa vipaji hautegemei chochote isipokuwa mapenzi ya anayepeana vipaji hivyo, Mungu.Binadamu anaweza kuwa na vipaji tofauti tofauti; kucheza densi, kuandika, kuimba, kucheza kandanda, kusuka, kuogolea, kuigiza na kadhalika.

Tukijikita kwenye mfano mmoja wa kuimba, wapo watu waliojaaliwa kipawa cha kuimba, yaani wasanii. Hata hivyo sio wote wanaoimba ni wasanii, wengine badala ya kujaaliwa vipaji, wamejaaliwa kubambanya na kulazimisha vipaji. Hawa tunawajua. Wapo na mifano yao pia ipo.

Katika kipawa cha kuimba, leo nataka tumzungumzie msaanii mmoja mwenye kipaji kikubwa sana cha kuimba, Mr Bado. Mr Bado ni msanii aliyezaliwa janibu ya pwani ya Kenya. Alizaliwa Kijiji cha Sita kilicho kaskazini magharibi mwa mji wa Watamu. Mr Bado alianza kuimba zamani sana baada ya kugundua kuwa ana kipaji cha kuimba alipokuwa kijana mdogo. Unapaswa kujua hata hivyo takribani familia nzima ya kina Mr Bado wamejaaliwa ama kipaji cha kuimba ama chochote kinachohusiana na kipawa cha kuimba. Kutegemea hili, tunaweza kusema kuwa kipaji kipo nyumbani kwao.

1712645989429 1
Msanii Mr Bado

Kipaji cha Mr Bado hata hivyo ni cha pekee na cha ajabu sana. Mola kamtunuku kwelikweli. Sijapata kuona msanii mwenye uwezo wa kuimba zaidi ya mitindo minne ya nyimbo kama alivyo BadoSasa hivi amejikita zaidi katika uimbaji wa Mwanzele ambazo ni nyimbo za kitamaduni kutoka jamii ya Wagiriama. Ufundi wake katika kuimba nyimbo hizi ni mkubwa mno. Unaweza kujua hili kupitia uteuzi wa maneno katika nyimbo hizo, kiimbo chake na mahadhi ya nyimbo zenyewe. Yaani kila kitu kinachohitajika katika uimbaji kipo barabara kwake, Mashallaah!

Usichojua ni kuwa, Mr Bado anaweza kuimba katika ubora uo huo nyimbo za *Taarabu* , nyimbo za *Bongo* *Flavour* , *reggae* na hata nyimbo za *Siasa* . Upekee wake na maajabu ni kwamba, ukimsikiliza akiimba taarabu unaweza kusema ni msaa wa nyimbo hizo, ukafanikiwa kumsikia akiimba Bongo Flavour utasema ni mzawa wa Tanzania hasa, ukimsikia akiimba Reggae ndio basi. Zaidi ukafanikiwa kumsikia akiimba nyimbo za Mwanzele na ukawa waijua lugha, walahi utapenda. Mr Bado anajua zaidi za ziada na yeyote anayejua usanii na matakwa yake anafaa kumvulia kofia.Huenda ikawa jina lake halijatamba na kutaratamba Kenya nzima, nahisi kabisa kuwa Kenya nzima hakuna msanii mwenye kipaji cha pekee kuliko Bado. Kutambuliwa kote Kenya ni bahati na kila mja ana bahati yake kutegemea majaliwa ya Mola mwenyewe.

You may also like

3 comments

Elvis Mweni Bokole April 9, 2024 - 7:36 am

Hongera sana kaka kwa kazi yako nzuri Mungu akuzidishie upande kwa hatua nyingne

Reply
Elvis Mweni Bokole April 9, 2024 - 7:39 am

Keep it up the good work brother

Reply
Ibrahim Mohamed April 9, 2024 - 8:45 pm

Good work

Reply

Leave a Comment

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?