Duniani, zipo sehemu nyingi hatari zinazotisha na kuogofya. Inahitaji ujasiri mkubwa na moyo mgumu zaidi kuzuru japo sehemu kadhaa yazo.Haidhuru lakini, inatoa ithibati tosha za ukuu na utukufu wa Mweyezi Mungu. Makala hii imekuandalia maeneo hatari kumi zaidi duniani kuyatembelea. Hasa ukiwa na woga wa kunguru.
1.Kisiwa Cha Nyoka( Snake Island)
Takribani maili ishirini na tano ( 25 ) kutoka pwani ya Brazili, Kipo kisiwa kinachojulikana kama ” The Snake Island). Kisiwa hiki kinachotisha na kuogofya pia kinaitwa Ilha da Queimada Grande kwa lugha ya Kibrazili. Inasemekana kuingiza mguu katika kisiwa hiki ndicho kitu hatari zaidi kukifanya kiasi kwamba serikali ya Brazili yenyewe imeweka marufuku kwa mwananchi yeyote kuingia katika kisiwa hiki kutokana na wingi wa nyoka wenye sumu kali. Idadi ya nyoka katika kisiwa hiki inasemekana kuwa nyoka watano katika kila mita Moja za mraba. Duru zinasema kuwa mvuvi wa mwisho aliyekwenda karibu na kisiwa hiki alipatikana siku chache baadaye ndani ya dau lake akiwa ameaga dunia.
2.Njia Ya Kifo( Death Road Road)
Njia hii inayojulikana pia kama North Yungas ama “Death Road ina kila sababu ya kuifanya sehemu hatari kutembelea duniani. Kusafiri juu ama chini ya njia hii yenye urefu wa Kilometre sitini na tisa (69) ni hatari zaidi kutokana na ukungu, mabonde na maji yasiyokoma kutiririka kutoka sehemu za juu za milima katika kila kona. Njia hii imesonga moja kwa moja na kukaribia msitu wa Amazon huku ikiwa imezungukwa na milima katika kila upande. Historia inasema kwamba kufikia mwaka wa 1994, takribani madereva mia tatu (300) walikuwa wameuawa katika kila mwaka
3. Bonde la Kifo ( Death Valley)
Katika mpaka wa California na Nevada, liko bonde linalojulikana kama the “The Valley of Death”. Hii ni mojawapo wa sehemu zenye joto Kali zaidi duniani. Rekodi ya joto kali kuwahi kurekodiwa katika Bonde la Kifo ama the Valley of Death ilikuwa Julai mwaka wa 2018 iliporekodiwa nyuzi joto 53 na nyuzi joto 42 mchana na usiku mtawalia. Wasafiri kadhaa kati ya mwaka 1849-1850 walipotea katika bonde hili. Ijapo mmoja ndiye aliyeaga dunia, walidhani kuwa bonde hilo ndilo lingekuwa mwisho wa maisha yao na walipopata nafasi ya kutoka nje, mmoja wao alilitazama na kusema , “Kwaheri bonde la Kifo” ndipo kubuniwa kwa jina hilo.
4. Skeleton coast ( Pwani ya Mifupa)
Kusini mwa Angola kunapatikana sehemu hatari kutembelea duniani inayotapakaa hadi kaskazini kwa nchi ya Namibia. Sehemu hii imeanza kutoka kusini mwa Mto wa Kunene hadi Mto wa Swakop. Sehemu hii ni hatari kutokana na hali mbaya ya hewa inayopatikana hapa. Joto kali, kukosekana kwa chakula na maji kunaifanya sehemu hii kimya kuwa hatari kutembelea.Eneo hili pia limejaa mifupa ya viumbe mbalimbali kama vile nyangumi, ndovu na kasa inayoipatia sehemu hiyo mazingira ya kutisha. Uvamizi wa majambazi na majangili unachangia zaidi kutisha kwa Pwani hii ya Mifupa.
5. Gates of Hell( Malango ya Jehanamu )
Katikati mwa jangwa la Karakum nchini Turkmenistan, ipo sehemu inayojulikana kama Darvaza Gas Crater ama “Gates of Hell”. Hii ni pango iliyo ndani ya ardhi iliyojaa gesi. Wanasayansi walitia pango hilo moto ili kuzuia kusambaa kwa gesi hiyo nje na tangu hapo moto mkali umekuwa ukiwaka kutoka mwaka wa 1971. Wakaazi wanaoishi karibu na hapa walilipa eneo hili jina Mlango wa Jehanamu kutokana na mlipuko na moto mkali unaopatikana katika pango hili lenye kipenyo cha urefu wa futi mia mbili thelathini ( 230 ).
6. North Sentinel Island( Kisiwa cha Kaskazini mwa Sentinel )
Sehemu hii inapatikana katika visiwa vyabAndamana, Andaman Islands. Sehemu hii inatambuliwa kama mojawapo wa sehemu hatari duniani kutembelewa na watalii. Wenyeji wa hapa wanaishi katika njia za kizamani na wamekataa kabisa njia zote zinazowezekana kujihusisha na Dunia ya sasa. Watalii wanapoingia hapa, wenyeji hapa huwapiga kwa kuwadhani kuwa watu wabaya. Wakazi wa kisiwa hiki hawazingatii mambo ya afya na watalii huenda wakabeba magonjwa wanapotembelea kisiwa hiki.
7. Madidi National Park. ( Hifadhi ya Madidi)
Pembezoni mwa Mto Amazon, inapatikana sehemu hii iliyotapakaa takrinani kilomita elfu kumi na tisa ( 19) za mraba. Ikiwa ndani ya msitu mkubwa, sehemu hii imesheni aina zote za miti na wanyama wa kutisha. Baadhi ya miti hapa ni hatari katika maisha ya binadamu. Msitu wa eneo hili unalindwa vikali na watalii hawaruhusiwi kuzuru peke yao kutoka na ndege, miti na wanyama wakali wanaopatikana hapa.
8. Ziwa Natron ( Lake Natron )
Kaskazini mwa Tanzania kunapatikana ziwa Natron. Ziwa hili halina tofauti na ziwa la moto kutokana na kiwango kikubwa cha chumvi kinachofanya maji yake kuwa hatari na yanayoweza kuchoma ngozi ama macho. Ziwa Natron limejaa bakteria wekundu. Ingawa viumbe vingi haviwezi kustahimili moto mkali wa maji ya ziwa hili yenye kiwanyo cha nyuzi joto mia moja ishirini, bakteria hawa wamelifanya ziwa hili kuwa makazi yao hali inayopelekea ziwa hilo kuwa tishio.
9.Oymyakon
Hiki ni kijiji kidogo kinachopatikana nchini Urusi( Russia ). Sehemu hii inatambulika kuwa hatari zaidi kwa sababu ya hali yake ya hewa. Baridi kali inayopatikana hapa huchangia hatari ya watalii na wasafiri kuzuru eneo hili. Kiwango cha baridi kinaweza kushuka hadi nyuzi hasi 40 ( -40 °C ), mara arobaini zaidi ya ubaridi wa barafu. Watu hawatembelei kijiji hiki kwa sababu hakuna miche inayopatikana hapa na hakuna mimea inayoweza kupandwa ikamea, hali inayofanya kukosekana kwa chakula kuwa tatizo kubwa. Takribani watu mia tano tu ( 500 ) wameishi na kustahimili makali ya kijiji hiki.
10. Jangwa la Danakili ( Danakil Desert )
Orodha yetu ya sehemu hatari zaidi kutembelea duniani inakamilishwa na jangwa hili. Jangwa hili linapatikana nchibi Ethiopia. Viwango vya joto katika jangwa hili aghalabu havishuki chini ya nyuzi joto 50 ( 50 °C ). Ngozi yako inaweza kubadikika hata kwa muda mchache wa kuishi katika jangwa hili. Hii ni kutokana na kiwango kikubwa cha mvuke wenye sumu kali unaopatikana hapa. Volkano inayopatikana hapa husababisha mlipuko wa mara kwa mara, hali inayolifanya jangwa hili kuwa mojawapo wa maeneo hatari kutembelea duniani.
Hizi ni baadhi ya sehemu kidogo kati ya nyingi sana zilizo hatari duniani. Makala hii inanuia kukupa mshawasha wa kujua mengi kuhusu dunia na kuanza utafiti wako. Soma na utupie maoni sehemu gani imekusisimua zaidi . Wasalaam.