Mlinzi kisiki wa Mashetani Wekundu wa Manchester United amerejea mazoezini. Luke Shaw amerejea mazoezini baada ya kukaa mkekani kwa takribani miezi mitatu. Shaw anayetambulika sana kwa uchezaji wake wa kukaba na kupiga pasi zinazozalisha mabao amekosekana kwa muda katika kikosi cha Erick Ten Hag na kuifanya klabu hiyo kuyumba katika baadhi ya michuano muhimu iliyosakatwa na Mashetani hao wekundu wa Old Trafford. Kukosekana kwake kuliifanya Man United kupokea vipigo kadhaa mikoni kwa watani wao wa jadi Manchester City, Brighton na New Castle United. Kujerea kwake kutaipa nguvu kubwa Man United kunyang’anyira kipute hicho cha Ligi kuu nchini Uingereza.
Kurejea kwa mlinzi huyo kunaipa Manchester United afueni baada ya kusuasua kufuatia majeraha kadhaa yanayoikumba timu hiyo, majeruhi wakiwa mlinzi wa kati na tegemezi Lisandro Martinez. Shaw anasifika sana kwa kujiamini, muda mwingi akipanda na kumsaidia winga Marcus Rashford pembezoni kushoto.
Akizungumza na vyombo vya habari, mkufunzi Ten Hag amesema kwamba Luke Shaw amekuwa mazoezini kwa muda wa wiki mbili na ana imani kuwa huenda akapatikana katika mtanange wa Jumapili watakapokipiga na Everton ugenini katika uga wa Goodison Park.